
Kamati Kuu ya CCM imefuta matokeo ya kura za maoni katika Jimbo la Handeni, mkoani Tanga ambako Omar Abdallah Kigoda ambaye ni mtoto wa mbunge wa zamani, marehemu Abdallah Kigoda alikuwa ameshinda.
Akizungumza
jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa
kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, uchaguzi wa kura maoni katika
jimbo hilo unarudiwa leo.
Alifafanua
kuwa wagombea 11 waliwania nafasi hiyo lakini wawili kati yao, Kigoda
na Hamis Amad Mnondwa walipata kura zaidi kuwashinda wenzao.
Mkutano
mkuu wa jimbo la Handeni, ulimchangua Omari Kigoda kwa kura 296
akiwashinda wenzake wawili Hamisi Mnondwa na Athumani Lukoya waliokuwa
wamechujwa kutoka miongoni mwa wanachama 11 walioomba nafasi hiyo.
“Lakini
matokeo yanaonyesha hakuna mshindi aliyepata kura za kuridhisha kuingia
katika ushindani na vyama vingine, ndiyo maana Kamati Kuu imeamua
urudiwe,” alisema bila kutaja idadi ya kura walizopata wagombea hao.
Mchakato
huo wa kupata mgombea unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea
ubunge wa jimbo hilo, Dk Abdallah Kigoda kilichotokea Oktoba 12, mwaka
huu nchini India.
Nape
alisema marudio hayo ya kura za maoni yatasimamiwa na makada watatu wa
CCM, Dk Maua Daftari, Dk Emmanuel Nchimbi na Abdallah Bulembo.
Nape
alisema Kamati Kuu inaendelea na kikao chake cha siku moja ambacho kina
ajenda ambazo hakutaka kuzitaja. Kamati Kuu imefanya uamuzi huo huku
kukiwa na sintofahamu juu ya chama hicho kuanza ‘utaratibu mpya’ wa
kuwateua watoto wa vigogo wa chama hicho wanaofariki dunia wakiwa
wabunge au wagombea, kuwania nafasi iliyoachwa na wazazi wao.
Mbali
na Omary, Goodluck Mtinga, mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utumishi) Celina Kombani naye amepitishwa na chama hicho kugombea
ubunge katika jimbo la Ulanga.
Utaratibu
kama huo ulitumika katika Jimbo la Kalenga mwaka 2014, CCM
ilipomsimamisha Godfrey Mgimwa, mtoto wa marehemu Dk William Mgimwa,
kugombea ubunge katika jimbo hilo lililokuwa likishikiliwa na baba yake.
Mwaka
2012, CCM pia ilimteua Sioyi Sumari kugombea ubunge katika Jimbo la
Arumeru Mashariki kuziba nafasi iliyoachwa na baba yake, marehemu
Jeremiah Sumari.

Post a Comment