Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya
Siasa kushiriki chaguzi zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini
ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka 2016 uliotangzwa na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC).
Kwa
mujibu wa barua iliyotolewa kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na Jaji
Mutungi ilieleza kwamba, kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya
258 inasisitiza vyama vya siasa kushiriki katika chaguzi zote
zinazotangazwa na tume za uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika
dola.
“Katika
nchi kidemokrasia na kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya
kidemorasia ya vyama vingi vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha
siasa kufikia malengo yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.
“Ni
wajibu wa kila chama cha siasa nchini kama wakala wa kukuza
demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii
matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka husika .
"
Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa njia moja au
nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia stahiki na
inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea uchaguzi, bali ni
vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha
Msajili huyo amesema kwa mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la
hiari kwa chama kushiriki uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda
sanjari na umuhimu wa kila chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na
tume ya uchaguzi.
“Hivyo
ni muhimu basi kila chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha
uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua
uhai wake katika mtazamo wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.
Aliongeza
kwamba hivi sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa
vimeimarika, hivyo sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au
kujiua kisiasa kwa kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya
hivyo.
Post a Comment