Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya
nne, Ezekiel Maige, jana alitajwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard Murunya ambaye ameshitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige anadaiwa kulipiwa nauli ya safari ya nje na
mamlaka hiyo kwa idhini ya Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika
Mashariki.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Sezari Semfukwe, alidai kuwa
Murunya na aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo,
Shad Kiambile, waliidhinisha malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa fedha
hizo zilikuwa kwa ajili ya safari ya Maige na msaidizi wake aliyetajwa
kwa jina la E. Muyungi na Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa mamlaka hiyo, alidai kuwa
Murunya na Kiambile, ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo
hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Hamidu Sembano, akisaidiana na
Rehema Mteta, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia
Kisinda, Semfukwe alidai kuwa utaratibu wa maombi ya safari, unatokana
na maelekezo ya mkuu wa idara na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi
na kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai kuwa aina zingine za safari zinahusisha
watu wa nje ambao, si waajiriwa wa NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au
shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi ya malipo namba 309/0238 ya Septemba
9/2011, ambayo ilikuwa na dokezo la safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa
Mkuu wa Kitengo cha Fedha. Pia alitoa hundi ya malipo nyingine
iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola zaMarekani 66,890 kwa kampuni ya
Wakala wa Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa hundi za malipo namba 310/0379 ya Oktoba 29,
2011 na ankara namba 5609 ya Septemba 7, 2011 zililipwa kwa Antelope
Tours & Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na Maige
kwa malipo ya dola za Marekani 66,890 (zaidi ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa kumbukumbu ya kitabu cha malipo ya hundi
inaonyesha hundi namba 002758 na 002755 za Septemba 9, 2011 zililipwa
kwa kampuni ya Cosmas Travelling Agent na zilitiwa saini na Kiambile na
Murunya.
Hata hivyo, wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo mahakamani
hapo ili vitumike kama ushahidi, malumbano ya kisheria yaliibuka baina
ya mawakili wa pande zote.
Malumbano hayo yaliibuka baada ya upande wa washtakiwa, ukiongozwa
na wakili Amani Mirambo, kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina
gani ambavyo upande wa mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha malumbano ya kisheria hivyo kumfanya hakimu
kuahirisha kesi kwa dakika 10. Baada ya muda huo, alirejea mahakamani
baada ya dakika hizo na kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande zote mbili, kutokana na malumbano ya
kisheria, Hakimu alikatizwa na Wakili wa Serikali Hamidu Simbano,
aliyemwomba kuahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe nyingine ya
washtakiwa kusomewa maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Rehema Mteta, aliwasomea maelezo ya awali juu ya
tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha mamlaka hiyo
kupoteza dola 66,890 (Sh. 133,780,000).
Mteta aliwataja washitakiwa, mbali na Murunya na Kiambile, kuwa ni
Meneja Utalii wa mamlaka hiyo, Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Cosmas Travelling Agent.
Post a Comment