MKAZI
wa kitongoji cha Kazima – Kichangani Kata ya Kawajense, Manispaa ya
Mpanda mkoani Katavi, Emmanuel Joseph (31) amemfanyia unyama mtoto wake
wa kumzaa, George Emmanuel (4) kwa kuvichoma kwa moto vidole vyake vya
mkono wa kushoto, akimtuhumu kukomba mboga yote ya majani aina ya
‘chainizi’ yenye thamani ya Sh 500.
Inasemekana
baba huyo amekuwa akiishi na watoto wake watatu baada ya kuachana na
mkewe wa ndoa, Semsni Jahala (28) Machi mwaka jana.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Rashid Mohamed amethitibisha
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lilitokea juzi saa 12
jioni katika kitongoji cha Kazima– Kichangani.
Akisimulia
mkasa huo, Kaimu Kamanda Mohamed alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa kwa
mahojiano na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi
wa awali wa shauri lake kukamilika.
“Jioni
hiyo ya tukio saa kumi na moja jioni mtuhumiwa huyo (Emmanuel) alipika
chakula cha jioni, ugali na mboga za majani maarufu chainizi kisha
akakihifadhi chakula hicho jikoni na kuondoka … aliporudi nyumbani saa
kumi na mbili jioni ili kuandaa chakula cha jioni ndipo alipobaini mtoto
wake (George) amekomba mboga yote ya majani.
"Alikasirishwa
na kitendo hicho na kusababisha kumpiga kisha kumchoma moto vidole
vyake vitatu vya mkono wa kushoto na kumsababishia maumivu makali,” alieleza Kaimu Kamanda.
Kwa
mujibu wa mashuhuda kutoka eneo hilo la tukio, mtoto huyo alikimbizwa
katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako amelazwa kwa matibabu.
Akizungumzia
tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda,
Oscar Mkenda alisema mke aliamua kuachana na mumewe huyo baada ya
kuchoshwa na ukatili na unyanyasaji aliokuwa akifanyiwa, ikiwemo kupigwa
mara kwa mara bila sababu yoyote.
“Mtoto
George alikomba mboga hizo zote za majani baada ya kushinda na njaa
mchana kutwa kwani hata kifungua kinywa hakupa asubuhi… hivyo baada ya
baba yake kubaini mtoto wake George amekomba mboga zote, ndipo
alipochochea moto na kuukandamiza mkono wake wa kushoto na kuunguza
vibaya vidole vyake vitatu,” alieleza Mkenda.
Post a Comment