Featured

Loading...


Kesi ya aliyemtukana Rais Magufuli Facebook imeendelea leo Mahakamani


Kesi inayomkabili Isaac Abakuk ambaye anatuhumiwa kumtukana Rais John Magufuli kwenye ukurasa wake wa facebook imeendelea leo May 17 2016 kwenye Mahakama Kuu kanda ya Arusha ambapo ushahidi umekamilika na kesi itaanza kusiklizwa mfululizo kuanzia June 7 mwaka huu.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Augustino Rwezire anayesikiliza kesi hiyo amesema upande wa mashtaka umekamilisha ushahidi wake na mtuhumiwa ataendelea na dhamana hadi kesi hiyo  itakapoanza kusikilizwa

David Kafulila ashindwa kesi yake dhidi ya Hasna Mwilima mahakama kuu kanda ya Tabora


Mbunge wa zamani wa   Kigoma kusini (NCCR-MAGEUZI), David Kafulila ameshindwa kwenye kesi yake iliyokuwa ikisikilizwa mahakama kuu kanda ya Tabora kuhusu kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa CCM, Hasna Mwilima
 
Kesi hii ilifunguliwa katika mahakama kuu kanda ya Tabora na kuendeshwa  chini ya Jaji Ferdinand Wambari.
 
Katika kesi hiyo upande wa mlalamikaji (Kafulila) uliongozwa na mawakili Prof. Abdallah Safari, Tundu Lissu na Daniel Lumenyera, Ili hali upande wa mlalamikiwa (Husna) uliongozwa na wakili Kenedy Fungamtama pamoja na mawakili wa serikali upande wa mwanasheria mkuu.

Tiketi Za Treni Kununuliwa Kwa Njia Ya Mfumo Wa Kielektroniki

Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajia kuanza kutoa huduma ya uuzaji wa tiketi kwa abiria wanaotumia usafiri wa treni kwa mfumo wa kielektroniki lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kuweza kurahisha ununuaji wa tiketi hizo na kupunguza usumbufu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa wakati akijibu swali la nyongeza lililoihusu Wizara yake ambapo ametaja maeneo ambayo mfumo huo utaanza kufanya kazi ni pamoja na Mpanda mpaka Tabora, Kigoma mpaka Tabora.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mhandisi Edwin Ngonyani akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Sabreen Hamza lililotaka kujua kwanini TRL isianzishe mfumo wa uwakala wa tiketi ili kupunguza adha wanayoipata wakazi alisema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa treni katika Mikoa ya Kigoma, uuzaji wa tiketi katika Stesheni ya Reli Kigoma umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ulanguzi wa tiketi.

Amefafanua kuwa, ili kudhibiti ulanguzi huo, Kampuni ya Reli Tanzania iliamua kubadilisha utaratibu kwa kuuza tiketi siku za safari na kwa kutumia vitambulisho jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ulanguzi wa tiketi hizo.

Ameongeza kuwa, utaratibu huo umekuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafiri kulala stesheni au kuwalazimu kuamka alfajiri ili kuwahi tiketi hizo.

"Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili si kuanzisha mfumo wa uwakala ambao utaiongezea TRL gharama za uendeshaji, tatizo kubwa lililopo ni idadi ndogo ya safari za treni ambapo huduma inayotolewa hivi sasa haikidhi mahitaji halisi ya wananchi na hivyo kuwa na uhaba wa tiketi kwa abiria", alisema Mhe. Ngonyani.

Aliongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatarajia kuongeza idadi ya treni za abiria kwa njia ya Kigoma ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akutana Na Balozi Wa Tanzania Nchini Uingereza, Dkt. Asha- Rose Migiro


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana  na Balozi wa Tanzania  nchini Uingereza, Dkt. Asha – Rose  Migiro kabla ya mazungumzo yao  Ofisini kwake jijini Dar es salaam  Mei 17, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha – Rose Migiro  ofisini kwake jijini Dar es salaam Mei 17, 2016.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mkenya Auawa na Polisi Kwa Kipigo .....Walikuwa Katika Maandamano Kutaka Tume ya Uchaguzi Iundwe Upya

Kijana mfuasi wa muungano wa upinzani nchini Kenya(CORD), Ben Ngari aliyeshambuliwa kinyama na polisi jana amefariki dunia kwa sababu ya majeraha yaliyompata
 
Wafuasi wa CORD jana waliandamana kushinikiza kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi (IEBC)

==> Tazama video ya Kipigo

Bunge laitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeshauri Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ili kuisaidia Bandari ya Dar es salaam kukabiliana na ushindani kutoka bandari ya nchi jirani.

Hatua hii itasaidia kuleta maendeleo ya haraka hapa nchini kupitia upokeaji na usafirishaji wa  mizigo mingi ya nchini na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Profesa Norman Sigala wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka ujao wa fedha.

Amesema kuwa nchi nyingine za wanachama wa Afrika Mashariki zinaendelea kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge kutoka Mombasa kupitia Nairobi , Kampala hadi Kigali kwa kasi kubwa.

Mhe. Profesa Norman alisema kuwa ili Bandari za Tanzania ziweze kushindana na Bandari za Kenya katika kupokea mizigo ya nchi za Uganda na Rwanda ni vema reli ya kati ikajengwa kwa kiwango cha standard gauge ili iziunganishe nchi hizo na reli inawezesha kusafirisha mizigo bila vikwazo.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa reli kwa kiwango hicho itasaidia kuwanufaisha mikoa 15 ya Tanzania bara.

Profesa Norman alisema kuwa ni vema Serikali ikaharakisha ujenzi wa reli ya kati na matawi yake yote ambayo ni kutoka Dar salaam kwenda kigoma, Uvinza hadi Msongati kwa ajili ya mizigo ya Burundi.

Alisema kuwa tawi jingine ni lile la kutoka Tabora hadi Kalemi kwa ajili ya mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na ile ya kutoka Tabora kupitia Shinyanga hadi Mwanza kwa ajili ya Ukanda wa ziwa.

Kwa upande wa Msemaji wa Kambi Rasmi  ya Upinzani Bungeni Mhe. James Mbatia akiwalisha maoni ya Kambi hiyo alisema kuwa reli ya kati ikiboreshwa itasaidia kutawala soko la usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kama vile DRC, Burundi , Uganda na Rwanda.

Alisema kuwa hivi sasa watanzania wanatakiwa kuwa na reli ambayo itaendana na hali  ya sasa inayowezesha usafirishaji wa mizigo kwa kasi na uwezo mkubwa wa kubeba mzigo mzito.

Mhe. Mbatia alishauri kuwa ili kufupisha ujenzi wa reli hiyo ni vema kukawa na wakandarasi ambao watapewa vipande vidogo vidogo vya takribani kilometa 200 ambavyo vitajengwa kwa wakati.

Naye Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli(RAHACO) inaendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya reli ili kuongeza uwezo wa njia zilizopo za reli ya kati za kubeba mizigo mizito zaidi.

Alisema kuwa mara baada ya kukakamilisha uboreshaji wa reli hiyo kutasaidia uhimilivu wa  mwendo kasi wa juu na kupunguza ajali za treni.

Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha shilingi 4,895,279,317,500.00 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha ujao.

Kati ya fedha hizo shilingi 2,212,141,496,500.00 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, shilingi 2,587,333,762,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi na shilingi 95, 804,059,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya mawasiliano.

Ripoti ya CAG Yaanika 'Madudu' Kibao Serikalini


Wakati Rais John Magufuli akipambana dhidi ya ufisadi, uzembe na ukwepaji kodi na uovu mwingine dhidi ya mali za umma, ripoti mpya ya ukaguzi iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha ana kazi kubwa zaidi kupata ushindi kwenye vita hiyo. 

Ripoti hiyo ya mwaka 2014/ 2015 iliyowasilishwa bungeni jana na CAG Mussa Juma Assad imeibua uozo zaidi kwenye halmashauri, taasisi za Serikali na mashirika ya umma, ikibainisha kuwa nchi ina tatizo kubwa zaidi ya watu ambao wamekuwa wakishughulikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano. 
 
Ripoti hiyo ya pili ya Professa Assad tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo mwaka juzi, imegusa taasisi zilizowahi kuwa chini ya Rais John Magufuli na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi Asha Rose Migiro, ambaye alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. 
 
Ripoti hiyo pia inaonyesha ufisadi katika ununuzi na uingiaji mikataba uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), matumizi yasiyo ya lazima kwenye Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jeshi la Wananchi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na mkoa wa Tabora. 
 
Pia ripoti hiyo imebainisha kuwa mapendekezo mengi ambayo CAG amekuwa akiyatoa kwa takribani miaka saba sasa, hayatekelezwi. 
 
Katika ripoti hiyo, CAG anaonyesha dosari kwenye utendaji wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa), na Wakala wa Barabara (Tanroads), taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambayo wakati huo ilikuwa ikioongozwa na Dk Magufuli. 
 
Profesa Ndalichako alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), wakati NEC imeguswa na ripoti hiyo katika suala la mchakato wa kuandika Katiba upya ulioongozwa na Wizara ya Katiba na Sheria. 
 
Ripoti hiyo ya Profesa Assad pia imebainisha kuwa Deni la Taifa, ambalo hutokana na fedha zinazopowa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharimia matumizi ya Serikali, limekuwa kwa tofauti ya Sh7 trilioni. 
 
Tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana, Dk Magufuli amekuwa akitumia ripoti zilizopita za CAG kusimamisha kazi au kutengua uteuzi wa watumishi wa umma wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi, lakini amekuwa akikosolewa kuwa hajaweka mfumo wa kukabiliana na hali hiyo. 
 
Katika ripoti hiyo, CAG anasema Temesa ilinunua kivuko chenye kasi ndogo kuliko ilivyotarajiwa na hadi ulipokuwa unafanyika ukaguzi Agosti 2015, chombo hicho kilikuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya mwaka. 
 
“Kuhusu dosari katika ununuzi wa kivuko chenye thamani ya Sh7,916,955,000, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Umeme, mitambo na ufundi (Temesa) iliingia mkatabana M/s Johs.Gram-Hanssen Bergensgade 10, DK 2100 Copenhagen Oe Denmark wa ununuzi wa kivuko cha Dar es Salaam –Bagamoyo chenye thamani ya Dola za Marekani 4,980,000 bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” anasema CAG. 
 
“Dosari zifuatazo zilibainika katika manunuzi hayo. Kasi ya kivuko haikuzingatia matakwa ya mnunuzi.  Ripoti ya mtaalamu wa ukaguzi ilibainisha kwamba kiwango cha juu na chini cha kasi ya kivuko wakati wa majaribio kilikuwa na kiwango kati ya knots 19.45 na knots 17.25 kinyume na makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba wa kasi ya kiwango cha 20,” anafafanua.
 
“Pili kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano Novemba 17, 2014 baada ya ucheleweshwaji wa siku 16; Pia nilibaini kwamba mpaka wakati wa ukaguzi, Agosti 2015, hati ya makabidhiano ilikuwa haijatolewa na mzabuni.” 
Ununuzi wa feri hiyo uliwahi kuzua sakata bungeni huku wabunge wa upinzani wakilalamika kwamba kilikuwa bomu kwani kinatumia zaidi ya saa tatu kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo badala ya dakika 45 za gari. 
 
Eneo jingine lililoguswa na CAG ni la malipo yaliyofanywa na Tanroads kwa makandarasi waliomaliza kazi zao. Kwamba moja ya matatizo makubwa ya taasisi hiyo ni udhaifu katika menejimenti. 
 
“Wakala wa Barabara (Tanroads) iliingia mikataba mbalimbali ya ujenzi wa barabara na madaraja. 
 
"Wakati wa ukaguzi nilibaini kwamba baadhi ya mikataba haikukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kuchelewa kwa ulipaji wa fedha. 
  
"Pia, nilibaini kwamba ucheleweshwajiwa malipo ya kati ya mikataba 16 ulisababisha ulipaji wa riba kiasi cha Sh 5,616,652,022 na Dola za Marekani 686,174.86,” alisisitiza CAG. 
 
Profesa Assad amezungumzia pia ukaguzi maalumu alioufanya kuhakiki fedha zilizowahi kutolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa taasisi mbalimbali zilizoko chini yake. 
 
Ukaguzi huo ulifanywa kutokana na ombi lililowasilishwa na katibu wa Bunge kwa barua yenye Kumb. NaCBC.155/188/01/26 ya Desemba 19, 2013. 

Bunge lilitaka kujua kama fedha zilizotolewa na wizara hiyo kwenda idara na taasisi zilizo chini yake zilipokewa na kutumiwa na wahusika kama ilivyopangwa. 
 
Katika ukaguzi huo, CAG alibaini kasoro katika vitabu vya akaunti za fedha vya Necta mwaka 2010, Sekretarieti ya Elimu ya Jumuiya ya Madola, Chuo Kikuu Huria (OUT), na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (Adem). 
 
“Udanganyifu wa malipo ya Sh185,350,000 yaliyolipwa Necta. Aprili 2010 kiasi cha 185,350,000 kilitumwa Necta kama matumizi ya kawaida. Wakati wa ukaguzi ilibainika kuwa kiasi hiki cha fedha hakikuandikwa kwenye vitabu vya uhasibu vya Necta. Hata hivyo, ilibainika kuwa stakabadhi ya mapokezi ya fedha hizo iliyotolewa na watumishi wasio waaminifu wa Necta ilikuwa ya kugushi,” anasema. 
 
“Kuhusu fedha zilizopelekwa OUT ni kwamba kati ya mwaka 2009/2010 Wizara ilihamisha Sh90,000,000 kwenda Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, ni kiasi cha Sh40,734,000 ambacho kilipokewa huku Sh49,266,000 hakijulikani. 
 
“Pia katika mwaka wa fedha 2010/2011 Wizara ilipeleka OUT Sh10,486,252,913 lakini ni Sh10,427,109,020 tu zinazoonekana kwenye vitabu huku Sh59,143,893 zikiwa hazimo kwenye vitabu.” 

Vilevile, CAG amesema katika ukaguzi huo Sh188, 838,528 zilizopelekwa Adem mwaka 2009/2010 zimeyeyuka. Mwaka huo Wizara ilipeleka Sh712,798,788 kwa taasisi hiyo, lakini vitabu vinaonyesha Sh523,960,260 zilipokewa na kurekodiwa, huku Sh188, 838,528 zikikosekana kwenye vitabu. 
 
Mbali ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya fedha, pia ameonyesha matumizi mabaya ya Sh7,080 milioni katika mchakato wa uchapaji Katiba Inayopendekezwa. 
 
“Katika ukaguzi wangu nilibaini kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ilipokea fedha kiasi cha Sh7,125 milioni kwa ajili ya kulipia gharama za kuchapisha vitabu vya Katiba Inayopendekezwa. 

"Kutokana na ufinyu wa muda, Wizara iliomba na kupewa kibali na Wakala wa Huduma za Manunuzi Serikalini kufanya manunuzi kwa njia ya dharura kupitia barua yenye kumbukumbu Na CAD.124/318/01/25 ya Desemba 11, 2014,” anasema CAG. 
 
“Katika ukaguzi wangu nilibaini vitabu vya katiba vilipokelewa kabla ya kuingia mkataba. Nilibaini kuwa mkataba ulisainiwa Februari 2, 2015, lakini vitabu vya katiba vilipokelewa Januari 26, 2015.” 

Ukaguzi uliofanywa Oktoba Mosi, 2015 umebaini kuwa nakala 158,003 za Katiba Inayopendekezwa zenye thamani ya Sh559,330,620 bado viko stoo au havijatumwa kwa wananchi ili vitumike kwa uhamasishaji. 
 
“Kwa hiyo, haikuwa rahisi kujua kama thamani halisi ya fedha ilipatikana na lini vitabu hivi vitasambazwa kwa walengwa. Pia, ilibainika kuwa vitabu hivyo havikujumuishwa kwenye Taarifa za Fedha za Mwaka husika,” anasema. 
 
Katika ripoti hiyo ya mwaka 2015/16, CAG Assad anasema ukaguzi wake umebaini matumizi ya mabilioni ya fedha katika ununuzi wa vitu visivyokuwa vya lazima au bila kuonyesha ushahidi wa malipo husika. 
 
Alibainisha matumizi ya zaidi ya Sh53 bilioni zilizotumiwa na taasisi sita pamoja na Sekretarieti mbili za mikoa katika mambo ambayo hayakuwa ya lazima, kama faini za kuchelewa kulipa kodi ya pango. 
 
Taasisi hizo ni Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na Mkoa wa Tabora. 
 
CAG Assad amebainisha matumizi ya ziada ya Sh109,722, 539 kwa ajili ya ununuzi wa gari aina ya Toyota Land Cruiser VX V8 kwa Sh297.5 milioni kutoka kampuni ya Toyota (T) badala ya kutumia mfumo wa ununuzi wa pamoja ambao ungefanya gari hilo lipatikane kwa Sh187.8 milioni. 
 
Alisema katika kipindi hicho, wizara 17, balozi mbili na sekretarieti za mikoa 11 zilitumia zaidi ya Sh11.3 bilioni bila kuwapo vielelezo vyovyote, hivyo kusababisha ashindwe kujua uhalali wa malipo hayo. 

==> Kwa taarifa zaidi, pitia  ripoti hizi za CAG
 
5. Ripoti ya Jumla ya Serikali za Mitaa 2014/2015

Breaking Newa: Rais Magufuli Aivunja Bodi ya TCRA na Kumsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Hiyo Dr Ally Yahaya Simba


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua  dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Aprili, 2016

Tanzia: Mke wa Rais Mstaafu wa Kenya Mama Lucy Kibaki Afariki Dunia


Mke wa Rais mstaafu  wa    Kenya, mama Lucy Kibaki amefariki dunia . Lucy alifariki katika hospitali ya Bupa Cromwell mjini London alikokuwa amelazwa.

Alisafrishwa hadi mjini Landon wiki moja iliopita kwa matibabu.

Akithibitisha kifo chake rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa kenya imesikitishwa na kifo cha mama Lucy mke wa aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki.

Katika taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari Uhuru amesema bi Lucy amekuwa mgonjwa kwa kipindi cha mwezi mmoja .

Amesema kuwa Kenya imempoteza mwanamke aliyechangia mengi katika maendeleo ya taifa la Kenya hususan katika vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Rais ametuma risala za rambi rambi kwa mtangulizi wake Mwai Kibaki pamoja na familia yake.
Chanzo:BBC

Polisi Dar Yakamata Ombaomba 45 Dar, 17 Wapelekwa gerezani


Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamewakamata na kuwaondoa ombaomba 45 na 17 wamewapeleka gerezani. 
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa Jamii, wanafanya utaratibu wa kuhakikisha watu hao wanarudishwa mikoani walikotoka. 
 
“Kazi hii inaenda vizuri na ombaomba wachache wamebakia ambao wakiwaona askari wanakimbia na kutokomea kusikojulikana,”alisema Sirro. 
Katika tukio lingine, Polisi wanawashikilia watuhumiwa 96 wenye umri wa miaka 15-18 wanaodaiwa kujihusisha na matukio ya kuvamia nyumba na kuiba usiku. 
 
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao wanajulikana kwa jina maarufu la ‘kumi ndani kumi nje’, walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya jiji na wanaendelea kuhojiwa na polisi, upelelezi utakapo kamilika watafikishwa mahakamani. 
 
“Watuhumiwa hawa wanavunja milango kwa mawe makubwa na kuiba televisheni na simu, upelelezi unaendelea na wanaendelea kutajana hivyo tutawakamata na wengine,” alidai kamanda huyo. 
 
Wakati huohuo, Kamanda Sirro alisema makosa ya kuvunja Sheria ya Usalama Barabarani mkoani hapa, yameliingizia jeshi hilo mapato ya Sh463 milioni kwa muda wa siku 10. 
 
“Jeshi la Polisi kazi yetu ni kusimamia sheria siyo kukusanya mapato, hivyo watu wazingatie sheria,” alisema kamanda huyo. 
 
Alisema ili kupunguza matukio ya uhalifu, jamii haina budi kuhakikisha kunakuwa na vikundi vya ulinzi shirikishi katika mitaa yao na Serikali za Mitaa zinapaswa kuhakikisha jambo hilo linazingatiwa na linafanyika.

Zitto Kabwe: Magufuli Hajagusa KANSA Ya Ufisadi


Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka Rais John Magufuli kukabiliana na vikundi vya mafisadi vinavyoiba mabilioni ya fedha za umma kupitia mikataba mibovu waliyoingia badala ya kuishia kutumbua majipu. 
 
Akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake jana, Zitto alisema ACT Wazalendo inaunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kupambana na ufisadi, lakini bado hajagusa kiini chenyewe. 
 
Zitto alitolea mfano wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa bado kuna kampuni inayolipwa Sh8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya mitambo yake ya umeme. 
 
Pia, alisema kashfa ya hati fungani imeongeza deni la Taifa kwa Sh1.2 trilioni. 
 
“Bado huo mtambo upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa Sh8 bilioni wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndivyo vikundi masilahi katika sekta ya nishati. Bila kuvibomoa, Rais ataonekana anachagua watu katika vita hii,” alisema Zitto. 
 
Alisema: “Ni kweli kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa rushwa ya Dola 6 milioni za Marekani zinazohusu hati fungani. 
 
"Serikali imewafikisha mahakamani madalali wa rushwa lakini waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani. Waliopokea rushwa ambao ni maofisa wa Wizara ya Fedha hawajashtakiwa.” 

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alisema vita ya ufisadi siyo ya kutumbua majipu tu, bali kujenga mfumo madhubuti wa kuzuia mianya ya rushwa. 
 
Alisema Rais Magufuli anapaswa kuwaongoza Watanzania katika vita ya kukataa mikopo kama hiyo ambayo inawasababishia umaskini. 
 
Aungana na hoja za upinzani 
Zitto alisema chama chake kinaungana na vyama vingine vya upinzani kwa hoja walizozitoa baada ya kutoka bungeni za kutokuonyeshwa moja kwa moja kwa matangazo ya televisheni kutoka bungeni, matumizi ya Serikali nje ya mpango wa bajeti na Serikali kutokuwa na mwongozo kwa mawaziri wake. 
 
Akizungumzia kusitishwa kwa urushaji wa matangazo ya Bunge, Zitto alisema hatua hiyo inatakiwa kupigwa vita kwa sababu inajenga udikteta katika nchi na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari za Bunge. 
 
“Ina maana TV zinapaswa kumuonyesha mtu mmoja tu akihutubia bungeni ambaye ni Rais tu... hapana hii siyo sawa,” alisema Zitto.

Akizungumzia suala la bajeti, Zitto alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka Rais kuhamisha fedha kwenda kufanya shughuli nyingine. Lakini alisema tangu Rais Magufuli achaguliwe, amekuwa akihamisha fedha wakati Bunge lilishapitisha bajeti. 
 
“Rais Magufuli kwani amekuwa waziri wa fedha, waziri wa ujenzi na Rais kwa wakati mmoja? Tunamtaka asiingilie majukumu ya mihimili mingine, wananchi tumnyooshee kidole na kumwambia afuate utaratibu,” alisema Zitto. 
 
Mbunge huyo pekee wa chama hicho, alisema tangu walipoapishwa, mawaziri hawajapewa mwongozo wa kazi na kutoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa miongozo kwa mawaziri. 
 
“Mpaka sasa nchi haina mawaziri kwa sababu hawajapewa miongozo. Kwa hiyo, Baraza la Mawaziri lina mawaziri wawili tu ambao ni Rais na makamu wake,” alisema Zitto na kulitaka Bunge kutengeneza mfumo wa kuisukuma Serikali kutekeleza mambo muhimu kwa Taifa. 
 
Kuhusu hali ya uchumi, Zitto alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka mpaka kufikia Sh29 trilioni lakini ana wasiwasi itakwama kwa sababu theluthi moja ya mapato ya ndani yanatoka bandarini ambako ripoti zinaonyesha kuwa yamepungua. 
 
Alisema Serikali imepanga kukopa Sh7 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti na kwamba hatua hiyo inazidi kuongeza deni la Taifa ambalo limelalamikiwa pia na Mkaguzi na Mdhibiti wa Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake. 
 
Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira aliwataka wajumbe wa chama hicho kusimama pamoja ili kukijenga chama hicho na kukifanya kiwe mbadala kwa Watanzania akisema kimewavutia watu wengi ambao wanachukizwa na ufisadi.

Deni la Taifa Lazidi Kupaa....Lafikia Shilingi Trilion 33. 5


Deni la Taifa limeongezeka kwa Sh7.05 trilioni, kutoka Sh26.49 trilioni Juni 30, 2014, hadi Sh33.54 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 27. 
 
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad, deni la ndani ni Sh7.99 trilioni huku deni la nje likiwa ni Sh25.55 trilioni.
 
Akiwasilisha ripoti hiyo jana bungeni, alisema kiwango hicho cha ongezeko la deni ni kikubwa katika kipindi cha muda mfupi. 
 
“Uchambuzi wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharimia madeni ya Sh4.6 trilioni mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo ya ndani ya Serikali ambayo ni Sh10.8 trilioni,” alisema. 
 
Alisema gharama hizo zikijumuishwa na gharama nyingine kama mishahara ya wafanyakazi na malipo ya likizo, Serikali hubaki na kiasi kidogo cha fedha za kugharimia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii. 
 
Profesa Assad alipendekeza mambo matatu kama sehemu ya mikakati ya kukabiliana na ongezeko la deni hilo, ikiwamo Serikali kuongeza jitihada za ndani za kuhamasisha ukusanyaji mapato ili kujenga wigo mpana wa kulipa madeni. 
 
Pia, alishauri kuwapo kwa mpango mkakati kuhusu fedha, hasa upunguzaji wa gharama na mikopo yenye masharti. 
 
Jambo la tatu, alishauri Serikali kuwa na uratibu mzuri wa shughuli zinazohusisha miamala ya fedha za kigeni, akisema hatua hiyo inawezekana kama kutakuwapo usimamizi thabiti.

Wafanyakazi wa TMA watakiwa kutumia mfumo wa kisasa kuhifadhi taarifa muhimu za ofisi


Watumishi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, (TMA) wametakiwa kuachana na mfumo wa zamani wa kutumia makaratasi katika kuhifadhi taarifa zao muhimu na badala yake kuanza  kutumia mfumo wa kisasa wa kieletroniki.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Pof. Makame Mbarawa  jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na wafanyakazi hao na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kununulia  karatasi.

“Katika ofisi zenu nimeona kila mtu anakomputa ni jambo zuri hivyo zitumieni katika kuhifadhi taarifa muhimu za taasisi yenu kwa mfumo wa kieletroniki” alisema Mhe.Prof.Mbarawa.

 Aliongeza kwa kusema kuwa serikali imetumia fedha nyingi katika kujenga mkongo wa taifa wa kuhifadhi taarifa muhimu  hususani za serikali pamoja na Taasisi zake hivyo ni budi  waanze kuutumia mkongo huo kwa kuhifadhia taarifa zao.

Pia aliongeza kwa kuwataka watumishi kuwa waadilifu,wachapaka kazi ,wabunifu na kuwa na uwazi baina ya watendaji wa juu na watumishi wa ngazi ya chini kwa kushirikiana na  wafanyakazi wa mikoani .

“Watanzania wanamatarajio mengi kutoka kwetu  katika kukuza uchumi wa nchi hivyo ni wajibu wetu kutimiza matarajio yao kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo miundo mbinu imara ya barabara, bandari ,shirika la ndege la kisasa na utabiri  wa hali ya hewa wenye uhakika ” alisema Mhe.Prof.Mbarawa.

Prof.Mbarawa  alitoa wito kwa kuwataka  watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano  kila mmmoja kujituma katika eneo lake la kazi ili kuleta matokeo yaliyobora na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa kufikia uchumi wa kati.

Mchina Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela Kwa Kuuza Bidhaa Bila Kutoa Risiti


Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh4.5 milioni, mfanyabiashara Huifang Ma baada ya kupatikana na hatia ya kuuza bidhaa na kushindwa kutoa risiti kwa kutumia mashine ya kieletroniki. 
 
Ma ambaye ni raia wa China na mkazi wa Mtaa wa Narung’ombe eneo la Kariakoo, alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukiri mashtaka mawili yaliyokuwa yakimkabili likiwamo la kushindwa kujisajili kulipa kodi ya ongezeko la thamani (Vat). 
 
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwanadamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Said Mkasiwa alisema kwa kuwa mshtakiwa alikiri mashtaka yanayomkabili, anatakiwa kulipa faini au kwenda jela miaka mitatu. Hata hivyo, Ma alilipa faini na kuachiwa huru. 
 
Katika hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa Machi 23, mwaka huu eneo la Karikaoo, mshtakiwa alishindwa kutoa risiti za kieletroniki kwa mteja wake. 
 
Ilidaiwa kuwa siku hiyo mshtakiwa ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya HM Textile Co Ltd iliyopo Mtaa wa Agrey, Kariakoo, alishindwa kutumia mashine za EFDs kwa ajili ya kutoa risiti kwa wateja walionunua bidhaa dukani kwake.
 
Kosa la pili, mshtakiwa alishindwa kujisajili kama mlipa kodi wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Ofisa wa TRA na Mfanyakazi Mmoja wa Yono Auction Mart Wafikishwa Mahakamani Kwa Rushwa


Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Mkwizu na mfanyakazi wa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Edward Magobela wamepandishwa kortini jana wakikabiliwa na mashtaka matatu ya rushwa. 
 
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh50 milioni na nyingine ya Sh5 milioni na kupokea Sh3 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Commercial Sales and  Services Tanzania Limited, Glenn Clarke. 
 
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lekayo alidai washtakiwa hao waliomba na kupokea kiasi hicho cha fedha ili kumwezesha mkurugenzi huyo kupunguziwa kodi aliyokuwa anadaiwa kutoka Sh375 milioni hadi Sh100 milion. 
 
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 
 
Hakimu Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo, aliwaeleza washtakiwa hao kuwa dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili. Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti na kupelekwa mahabusu. 
 
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 9 mwaka huu.
Awali, akiwasomea mashtaka, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo Aprili 19, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Namba 7 ya mwaka 2011. 
Katika shtaka la kwanza, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja na wengine ambao hawajakamatwa, waliomba rushwa Sh50 milioni kutoka kwa Clarke. 
 
Wakili Lekayo, alidai katika shtaka la pili washtakiwa hao kwa pamoja na wengine ambao hawajakamatwa bado, walijihusisha na vitendo vya kumuomba rushwa ya Sh5 milioni mkurugenzi huyo ili wampunguzie kodi kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni. 
 
Katika Shtaka la tatu, Wakili Lekayo alidai washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kupokea rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa Clarke ili wampunguzie kodi kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya April 7

Viongozi CUF washutumiwa kwa kukosa uzalendo


Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekishiutumu Chama cha Wananchi (Cuf) pamoja na viongozi wao kwa kukosa uzalendo kutokana na kauli zao za kuunga mkono wahisani kuisitishia misaada Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa kuteuliwa kutoka katika chama cha Ada-Tadea, Juma Ali Khatib ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa marudio, alipokuwa akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar kwenye baraza hilo mjini hapa.

Alisema, viongozi wa Cuf wameonesha udhaifu mkubwa wa kukosa uzalendo kwa kitendo chao cha kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa misaada kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema, Zanzibar ni nchi yenye kufuata katiba yake kwa hiyo ilikuwa na mamlaka kamili kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuitisha uchaguzi wa marudio baada ya kuufuta wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Nimesikitishwa na kauli za viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kuhusu uamuzi wa kususia misaada kwa Tanzania. Viongozi hao wameonesha udhaifu na kukosa uzalendo,” alisema Khatib.

Alisema chama chake kiliamua kuingia katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kwa sababu umeitishwa na chombo halali kwa mujibu wa katiba, chenye majukumu ya kusimamia uchaguzi kikiwa hakiingiliwi na mtu yeyote.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini , Machano Othman Said, alisema kitendo cha viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa kutoa misaada kwa Tanzania hakikubaliki hata kidogo kikionesha udhaifu mkubwa wa viongozi hao katika uzalendo wa nchi.

Watu Watano Wafariki Dunia Jijini Dar Kwa Kuangukiwa Na Kifusi.


Watu watano wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na kifusi na mti wakiwa wamelala, ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa karo la majitaka la nyumba ya jirani iliyo juu ya mlima.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa karo hilo na kwamba maji yaliyotoka kwa kasi yaling’oa mti, kifusi na kisha kuifunika nyumba ya jirani iliyojengwa bondeni na kusababisha vifo hivyo.

Alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri katika Mtaa wa Ukwamani Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, na waliokufa ni Ephraim Manguli (47), watoto wake Daniel Ephraim (5) na Frederick Ephraim (1). Wengine ni mjukuu wa mwenye nyumba hiyo, Greyson Clarence (3) pamoja na msichana wa kazi za ndani aliyetambulika kwa jina moja la Maria.

“Majeruhi ni pamoja na Emilia Nakiete (19) aliyejeruhiwa mkono wa kulia na kidevu na Fadhili Fariji (8) aliyejeruhiwa mguu wa kulia. Wengine watatu walitibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa. Majeruhi wawili bado wamelazwa na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo,” alisema Kamanda Fuime.

Baada ya kutafutwa, mmiliki wa nyumba hiyo Blandina Clarence Akilizao (49), alisema nyumba yake ilikuwa na wapangaji sita wenye familia, huku familia yake ikiwa na watu saba.

“Ndani ya nyumba nilikuwa na watoto wawili, wadogo zangu wawili na wajukuu wawili, pia kulikuwa na familia tano zilizokuwa na watu 17 jumla,” alisema mama huyo kwa uchungu.

Blandina alisema nyumba hiyo aliachiwa na mumewe aliyefariki dunia mwaka 2000 na kwamba hivi sasa hana msaada wowote, kwani akiba ya fedha aliyokuwa nayo kiasi cha Sh200,000 imefukiwa na kifusi na hajui namna ya kuipata.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mpangaji, Msafiri Nyamolelo alisema ajali hiyo ilitokea ghafla na kabla ya ukuta kuanguka, ulisikika mlipuko na baadaye kelele za maji, kisha kishindo kikubwa juu ya paa.

“Karo lilipasuka na kwa kuwa ardhi hiyo hapo juu kwa muda mrefu ni dampo lenye mifuko mingi, ardhi ilikuwa imeoza, hivyo miti mikubwa ambayo iliota huko iling’oka baada ya karo kupasuka na kutua juu ya paa la nyumba sambamba na udongo kutoka juu nao ukafunika,” alisimulia Nyamolelo.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Mtaa wa Ukwamani, Kata ya Kawe Kassim Mbezi alisema chanzo cha ajali ni kupasuka kwa karo la choo na maji yaliyomwagika ambayo yaliuzoa mti huo na kifusi kilisombwa na kuifunika nyumba hiyo.

“Tulipofika eneo la tukio tuliwakimbiza majeruhi wote Mwananyamala, lakini kwa bahati mbaya walifariki baada ya kufika mapokezi wote walitoka wakiwa bado wanahema, lakini ilipofika saa tatu asubuhi tukaambiwa kwamba kulikuwa na ‘house girl’ hivyo baada ya kufukuafukua tukaupata mkono na baadaye kuufikia mwili mzima, huyu tulimtoa akiwa tayari amefariki,” alisema Mbezi.

Mbezi alitoa wito kwa wakazi wa bonde hilo kuhama kwa kuwa gema bado linaonekana na ni hatari na changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na maafa kabla ya kutokea. 
© Copyright JICHO LETU
Back To Top